Psalms 60

Kuomba Kuokolewa

(Kwa Mwimbishaji: Mtindo Wa Shushani Eduthi. Utenzi Wa Daudi. Wa Kufundisha. Wakati Alipopigana Na Waaramu Kutoka Aramu-Naharaimu Na Aramu-Soba, Yoabu Aliporudi Nyuma Na Kuwaua Waedomu 12,000 Katika Bonde La Chumvi)


1 aEe Mungu, umetukataa na kutokea ghafula juu yetu,
umekasirika: sasa turejeshe upya!

2 Umetetemesha nchi na kuipasua;
uiponye mavunjiko yake, kwa maana inatetemeka.

3 bUmewaonyesha watu wako nyakati za kukata tamaa;
umetunywesha mvinyo unaotuyumbisha.


4 cKwa wale wanaokucha wewe,
umewainulia bendera,
ili iweze kutwekwa dhidi ya upinde.


5 dTuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume,
ili wale uwapendao wapate kuokolewa.

6 eMungu amenena kutoka patakatifu pake:
“Nitaigawa Shekemu kwa ushindi
na kulipima Bonde la Sukothi.

7 fGileadi ni yangu na Manase ni yangu;
Efraimu ni kofia yangu ya chuma,
nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala.

8 gMoabu ni sinia langu la kunawia,
juu ya Edomu natupa kiatu changu;
nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.”


9 Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome?
Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu?

10 hEe Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi,
na hutoki tena na majeshi yetu?

11 iTuletee msaada dhidi ya adui,
kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.

12 jKwa msaada wa Mungu tutapata ushindi,
naye atawaponda adui zetu.
Copyright information for SwhKC